Saturday, May 11, 2013

Utawala mpya

Pia inasemwa kwamba Moyes hajawahi kusafiri na timu kwenda hata jijini Milan kutetea ushindi. Zaidi ya yote, Moyes si kama Jose Mourinho.Akiwa kocha wa Everton, staili yake ya uchezeshaji ni nzuri lakini haihamasishi kusaka ubingwa.

WIKI hii kumekuwa na mlolongo wa matukio kwenye soka la kimataifa. Jumatano kocha, Alex Ferguson, alitangaza kujiuzulu na juzi Alhamisi kocha wa Everton, David Moyes, alipewa mikoba ya kuiongoza Manchester United.
Ferguson anasema kocha huyo ni mzuri na ataifikisha timu mbali, lakini wengi wanajiuliza iwapo Moyes ni thabiti kuongoza klabu hiyo na kama anaweza kupata mafanikio ya kocha huyo kutoka Scotland.
Kuna taarifa mbalimbali zinazosema kuwa Moyes hana sifa ya kuwa kocha wa Manchester United, kila mmoja anatoa sababu zake.Kinachoelezwa kwa Moyes ni kwamba, hakuwahi kutwaa vikombe wala kufundisha timu iliyowahi kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Hakuwahi kumnasa mchezaji wa dau linalofikia Pauni 30 milioni, hafahamu mipango ya kutengeneza mazingira ya kutwaa ubingwa katika hatua za mwisho wa ligi.
Pia inasemwa kwamba Moyes hajawahi kusafiri na timu kwenda hata jijini Milan kutetea ushindi. Zaidi ya yote, Moyes si kama Jose Mourinho.Akiwa kocha wa Everton, staili yake ya uchezeshaji ni nzuri lakini haihamasishi kusaka ubingwa.
Itakumbukwa katika msimu ambao Blackpool ilicheza kabla ya kushuka daraja, iliifunga Everton na kikosi cha Moyes kikamaliza nafasi ya saba.Kwa upande mwingine, Manchester United chini ya Sir Alex Ferguson ina kazi ya kusaka mabao tu. Katika misimu minane ya Moyes, nafasi ya Everton ilikuwa mbaya kutokana na kushindwa kutengeneza safu imara ya washambuliaji.
Walikuwa wa saba katika msimu wa 2010/11, lakini klabu 10 zilifunga mabao zaidi yao.
Walikuwa wa 11 msimu wa 2005/ 2006 na pia ni msimu ambao walifanya vibaya mno. Everton kwa sasa ipo nafasi ya sita na inaweza kumaliza hata nafasi ya saba.
Bado kuna maswali mengi, kwamba kweli Moyes ni kocha stahiki wa kumrithi Ferguson Manchester United?
Kwa nini inasemekana Man United ni kama imepotea kwa kuchagua jina la mtu ambaye nyota yake haijang’aa wakati kuna makocha wenye majina makubwa Ulaya kama, Carlo Ancelotti aliyewahi kuzinoa AC Milan, Juventus, Chelsea na Paris St-Germain?
Mwingine ni Mourinho aliyewahi kuzinoa Porto, Chelsea, Inter Milan na Real Madrid?

Ferguson ajibu
Hayo ni mawazo ya watu tu, lakini Alex Ferguson anaamini Moyes ana sifa zote za kuinoa Manchester United na siku zote alikuwa akimwaza kuwa ni mmoja wa makocha wanaoweza kumrithi. Ferguson alisema anatarajia makubwa kutoka kwa kocha huyo.
“Wakati tulipojadiliana juu ya nani anaweza kazi kwenye klabu hii, kila mtu alikiri Moyes ni mtu sahihi. Sidhani kama mtu yeyote ana swali juu ya kiwango chake. Atawapeleka puta wapinzani wake,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa Everton, Bill Kenwright, amekiri amempoteza kocha mahiri. Bill alisema kuwa kama angekuwa na nguvu ya kumzuia angemzuia, lakini hana uwezo huo na akaongeza kuwa amepata pigo kubwa.
Naye Moyes alisema anajiona mwenye bahati kuwa kocha mpya wa Manchester United.
Pia mkongwe wa Old Trafford, Sir Bobby Charlton, alisema David Moyes ni mashine mpya kwenye klabu hiyo. Mkurugenzi huyo aliongeza: “Nimewahi kusema nataka kocha mpya awe anaifahamu Man United. Moyes anafahamu cha kufanya.”
Baada ya kukubali kutua katika klabu hiyo kwa mkataba wa miaka sita Moyes alitamka: “Ni jambo la heshima kuona Ferguson akinichagua, ninaheshimu kila kitu alichofanya. Itakuwa ni kazi ngumu kufuata nyayo za kocha mzuri, lakini nitajitahidi.”

0 comments:

Post a Comment