Wednesday, October 24, 2012

Milovan awaondoa hofu mashabiki Simba

 
 
Kocha wa Simba, Milovan Cirkovic.
Na Khatimu Naheka
KOCHA wa Simba, Milovan Cirkovic, ameibuka na kuwaambia mashabiki wa timu hiyo: “Tulieni, sare zisiwape shida.”
Kauli hiyo ya Milovan inakuja kufuatia mashabiki wa timu hiyo kuonekana kukatishwa tamaa na sare tatu mfululizo kwenye michezo ya Ligi Kuu Bara.
Akizungumza na Championi Jumatano, Milovan alisema haoni sababu ya mashabiki wa Simba kuanza kuhofia matokeo hayo huku akidai yanatokana na kucheza kwenye viwanja vibovu na uamuzi mbaya.
Milovan alisema tayari kikosi chake mpaka sasa hakijapoteza hata mchezo mmoja zaidi ya sare nne ambazo wamezipata kwenye ligi, hivyo siyo kibaya hata kidogo.
“Sidhani kwamba ni sahihi kwao (mashabiki) kuchukia au kuumiza kichwa juu ya hizi sare, huu ni mpira, siyo kwamba tunapopata sare inamaanisha kwamba timu ni mbovu, tatizo kubwa ni viwanja vibovu, kwa staili yetu ya uchezaji ni vigumu kufanya vizuri kwenye viwanja hivyo lakini pia tatizo lingine ni uamuzi.
“Hatujapoteza mechi yoyote mpaka sasa, zaidi ya hizi sare ambazo ndani yake tumekuwa tukipata pointi moja, ambayo ni bora kuliko kupoteza kabisa, lakini bado tuna mechi nyingi sana mbele yetu, hata hawa tunaoshindana nao, wataendelea kukutana na matatizo tunayokutana nayo sisi,” alisema Milovan.
 

0 comments:

Post a Comment