Wednesday, October 24, 2012

WATUHUMIWA VURUGU MBAGALA, NI MAJUTO

 Na Musa Mateja, Dar es Salaam
WATUHUMIWA wanaokabiliwa na kesi ya kuharibu na kuchoma moto makanisa kwenye vurugu za waumini wa dini ya Kiislamu zilizotokana na mtoto kukojolea msahafu hivi karibuni, Jumatatu iliyopita  walipandishwa kizimbani na kusomewa mashitaka yao na wengi wao walionesha majuto baada ya kutupwa rumande.
 Watuhumiwa hao watano wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
 
Watuhumiwa hao watano, walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka matano na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Tumaini Kweka, yanayowahusisha na kesi ya kula njama kwa nia ya kutenda makosa kinyume na kanuni ya adhabu.
Makosa mengine yanayowakabili watuhumiwa hao ni pamoja na kuvunja jengo kwa nia ya kutenda makosa, uharibifu wa mali za kanisa, wizi wa vifaa vya kanisa, kuchoma kwa makusudi jengo lililotumika kwa shughuli za ibada na kumtishia mlinzi.
Watuhumiwa hao wakipandishwa mahakamani.
  Mashtaka hayo yamewakilishwa mbele ya Hakimu Binge Mashabala na kuwaomba washitakiwa kuthibitisha makosa hayo kama kweli waliyafanya ambapo kwa pamoja waliyakana, hali iliyomfanya hakimu huyo kuiahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 30 mwaka huu ambapo watafikishwa mahakamani hao kusomewa tena.
Washitakiwa wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Shabani Hamisi, Issa Abdullah, Kambi Haji, Hamadi Mahambo na Wajabali Julius, kwa mujibu wa Wakili Kweka, jumla ya mali wanazodaiwa kuharibu zinakadiriwa kuwa na thamani ya shilingi milioni 520.
Kufuatia kutupwa rumande kwa watuhumiwa ndugu na jamaa zao waliangua vilio mbele ya mahakama hiyo walipokuwa wakishuhudia washitakiwa wakipandishwa kwenye kalandinga tayari kwa kupelekwa mahabusu.


0 comments:

Post a Comment