Wednesday, October 24, 2012

Mbuyu Twite ashusha bonge la mchezaji Yanga


Mbuyu Ywite akiwa na kiraka Kabange Twite

DORIS MALIYAGA NA CALVIN KIWIA.
SAHAU kidogo kuhusu Mbuyu Twite ambaye Simba hawataki hata kumsikia.Yanga wamemshusha nchini kiraka Kabange Twite ambaye ni pacha wa Mbuyu tayari kwa mazungumzo ya usajili.

Mchezaji huyo ambaye yupo Dar es Salaam tangu juzi Jumapili, ataanza mazoezi na Yanga muda wowote kuanzia sasa na tayari vigogo wa Kamati ya Usajili chini ya Abdallah Bin Kleb wamekaa naye meza moja.

Katika kile kinachoonekana ni kuihofia Simba, Yanga wamempa ulinzi wa makomandoo mchezaji huyo kila anapokuwa na imekuwa ngumu kuchanganyika au kusalimiana na mashabiki kiholela.

Yanga imepanga kumsajili mchezaji huyo kwenye Dirisha Dogo la Usajili ifikapo Desemba, jambo ambalo linamaanisha mchezaji mmoja wa kigeni lazima achomolewe na kupewa chake ili kutoa nafasi kwa Kabange.

Yanga ina wachezaji watano wa kigeni ambao ni Yaw Berko (Ghana), Didier Kavumbagu (Burundi), Mbuyu (DR Congo), Hamisi Kiiza (Uganda) na Haruna Niyonzima (Rwanda).

Kabange ambaye ni kiraka kama ndugu yake amefikia nyumbani kwa pacha wake, Mbuyu anayeishi maeneo ya Kinondoni Mkwajuni. Alifika Dar es Salaam Jumapili akitokea DR Congo na aliishuhudia mechi ya Yanga dhidi ya Ruvu Shooting.

Licha ya kutotaka kutajwa jina na kutoa ufafanuzi wa kina, kiongozi mmoja mwenye maamuzi makubwa ndani ya Yanga jana Jumatatu alisema:

"Tuna mpango wa kumsajili kama mambo yatakwenda sawa. Unajua, Mbuyu na Kabange wamekuwa wakiishi pamoja kwa kipindi chote na walitengana baada ya yeye kuja Yanga."

"Hivi karibuni, Mbuyu hakuwa mtu mwenye furaha na alipenda ndugu yake huyo wawe pamoja kikosini kama unavyojua mapacha wanapenda kukaa pamoja na kilichopo sasa tunamsikilizia mwalimu (Ernest Brandts).

"Ataanza kwanza mazoezi ya pamoja na Yanga ili isionekane amesajiliwa kwa sababu ya matakwa ya ndugu yake lakini aonyeshe kiwango kwanza uwanjani. Mchezaji huyo atajiunga na mazoezi ya timu ili kocha aweze kumtathmini vizuri," alifafanua kiongozi huyo.

Hata hivyo, usajili wa Kabange ni rahisi kwani Brandts anamjua vilivyo, alikuwa naye APR ya Rwanda.

Kocha msaidizi wa Yanga, Fred Minziro amesema: "Kabange ni mchezaji mzuri, nasema hivyo kwa sababu namfahamu na nimeshamwona kwenye mashindano mbalimbali ikiwamo ya Kagame."

Mbuyu ameonyesha umahiri mkubwa kwenye kurusha mipira ndani ya Yanga utadhani anapiga kwa mguu.

Mchezaji huyo mwenye uraia wa Congo na Rwanda amepewa jukumu la urushaji mipira yote ya Yanga ambayo inakuwa karibu na maeneo ya lango la timu pinzani.

Mbuyu ana mapafu ya kurusha mpira umbali wa mita 25 hadi 30.

Beki huyo ghali aliiambia Mwanaspoti kuwa: "Nafikiri siri hapa ni kipaji Mungu amenipa. Sijawahi kufanyia mazoezi, suala la urushaji mipira."

Beki huyo mwenye uwezo pia wa kupiga mipira ya faulo tangu akabidhiwe jukumu hajarusha mpira uliozaa bao.

Urushaji mipira wa Mnyarwanda huyo umekuwa kivutio kwa mashabiki wa Yanga. Kila inapotokea timu hiyo imepata mpira wa kurusha hupiga kelele kumtaka arushe.

Unaweza kumfananisha na kiungo wa Stoke City, Rory Delap, ambaye ni gwiji wa kurusha mipira kwenye Ligi Kuu England.

Yanga imekuwa na ngekewa ya kupata nyota wenye mapafu ya kurusha mipira kwani awali alikuwapo beki Fredy Mbuna ambaye baadaye ilimtema akiwa ameicheza timu hiyo zaidi ya miaka kumi. Lakini pia alikuwapo Bakari Malima 'Jembe Ulaya'.

Tanzania pia imewahi kuwa warushaji tu wazuri wa kama beki wa zamani wa Simba, Mohamed Kajole na nyota wa zamani wa Yanga, Yussuf Ismail Bana na Godwin Aswile 'Scania'.

Akizungumza na Mwanaspoti, Minziro alisema: "Twite ni mrushaji mzuri wa mipira na mpigaji mahiri wa mipira ya adhabu na ndiyo maana anapewa nafasi kubwa ya kupiga.

"Sishangai uwezo wake huo hata alipofunga bao la faulo kwa Ruvu kwa sababu nilimwona akifanya hivyo akiwa na APR ya Rwanda," alisema Minziro. 

Mbuyu ambaye amekuwa akichezeshwa namba tofauti za ulinzi kama mbili, tatu, nne, tano na sita kikosini hapo na kuonyesha uwezo amekuwa tegemeo la Yanga kwa sasa akiwa tayari amefunga mabao mawili katika Ligi Kuu Bara.
 

0 comments:

Post a Comment